Sunday, May 11, 2008

Kijana ni nani?

Kutokana na tafsiri ya umoja wa mataifa (UN) kijana ni mtu wa miaka 15 hadi 24, angalia www.un.org/youth.
Neno kijana linatafsiriwa katika tafsiri tofauti katika kila jamii.Mathalan nchini Tanzania kijana ni mtu wa miaka 15 hadi 39, yaani baada ya baleghe.
Tukikiangalia kipindi hiki cha maisha kwa undani ni kipindi kizito katika maisha ya mwanaadamu.Mabadiliko makubwa ya kimaumbile hutokea sambamba na kukomaa kwa mawazo.Ni kipindi cha mpito kutoka utoto kuelekea uzee.Ni kipindi chenye heka heka nyingi kwa vijana kutokana na mabadiliko ya kimaumbile,kwani kijana hutaka kujionyesha kwamba yeye ni nani katika jamii.
Kwa kweli na hapa ndiyo msingi wa maisha ya uzeeni.Na pia ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa kwani vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa.
Kwa hiyo kama wewe ni mtu wa umri wa miaka 15 hadi 39 karibu tujadili.Hapa ni kwako.Tuonane kesho kuangalia nini jukumu la kijana katika jamii inayomzunguka.Je kijana ana wajibu gani?

Utangulizi

Masalkheri vijana wenzangu wote popote mlipo ulimwenguni.Karibuni katika maskani yetu tuweze kujadili kwa pamoja mambo yanayotusibu katika maisha ya kila siku na kuyatafutia suluhu.Ninaamini kwamba kwa pamoja tunaweza kwani what man did man can do, yaani alichoweza kufanya mtu hata mwingine nae anaweza.
Uwezo tunao,ila tunacho kosa bado hatujaweka nia au azma ya kuleta mabadiliko katika maisha yetu.Amka kijana mwenzangu,anza kuchukua hatua za kubadilisha maisha yako na wanaokuzunguka leo.Linalowezekana leo lisingoje kesho,kumbuka udongo uwahi ungali maji.
Raslimali ya mwanaadamu ni uzima wake,ukichezea ujana kumbuka fainali uzeeni.Mwili ukishazeeka na kukosa nguvu usitarajie kuja kuweza kufanya jambo uzeeni.Ukiufuja na kuuchezea mwili wako sasa,usijelia mgongo utakapokua haunyooki na viungo vimechoka kwa uzee.Kaa ufikiri kabla hujafikiriwa.Juta kabla hujajutiwa na lia kabla hujaliliwa.